Soma taarifa kwa umma iliyotolewa na uongozi wa DICOTA Aprili 19, 2020.

DICOTA imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza na kushiriki katika maswala ya afya nchini Tanzania. Mwaka 2017 na 2019, DICOTA iliunganisha wadau mbali mbali wa ndani na nje ya nchi katika makongamano maalum yaliyokuwa na nia ya kuwaunganisha wadau mbali mbali wa sekta za afya. Mikutano hii miwili iliyofanyika Washington DC, nchini Marekani na ilijumuisha zaidi ya washiriki mia mbili (200).

Baada ya janga la homa ya mafua ya COVID-19 kuanza, DICOTA ikishirikiana na taasisi mbalimbali, ilianza kuratibu majadiliano kupitia mtandao wa Zoom. Mijadala hii ilianza mwezi Machi na bado inaendelea. Mijadala hii imekuwa ikiwaungunisha wadau mbali mbali wa sekta ya afya, pamoja na watoa huduma wa kiTanzania na wenye asili ya Tanzania wanaojishughulisha katika nchi mbali mbali duniani. Hadi sasa, hii mijadala ambayo bado inaendelea imeweza kushirikisha watu zaidi ya mia nane (800).

DICOTA inapenda kuainisha mtiririko wa ushiriki wetu kwenye Kampeni ya Dhibiti Mlipuko: COVID-19 Tanzania, kama ifuatavyo:

  • Mnamo Aprili 3, wanachama wetu walipendekeza kwamba pamoja na majadiliano ya mtandaoni, DICOTA pia ichukue jitihada kuchangisha fedha taslimu kutoa msaada Tanzania. Siku hiyo hiyo, uongozi wa DICOTA ulifanya maamuzi kujumuika na kikundi cha diaspora ambacho kilikuwa kimeshaanza mipango ya kuratibu kampeni ya michango ya COVID-19.
  • Aprili 4, 2020, DICOTA iliombwa na kikundi hicho, ambacho sasa ni Kamati ya Dhibiti Mlipuko: COVID-19 Tanzania, kusimamia fedha zitakazochangishwa kupitia kampeni ya “Dhibiti Mlipuko: COVID-19 Tanzania”. DICOTA ilipokea na kukubali ombi hilo, na mara moja, akaunti maalum ya benki ilifunguliwa na kusajili namba ya simu rasmi kwa ajili ya Kampeni hii. Pia DICOTA ilikubali wajibu wa kusimamia upokeaji wa fedha zote, pamoja na kuhakikisha zinatumika kwa umakini kusaidia juhudi za kudhibiti janga la COVID-19 Tanzania.
  • Aprili 6, kabla ya kuzindua rasmi kampeni ya “Dhibiti Mlipuko COVID-19 Tanzania”, DICOTA iliwasiliana na kuutaarifu Ubalozi wa Tanzania hapa Marekani na Idara ya Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu juhudi hizi. Taarifa hiyo ilitolewa kwa nia ya kuutaarifu Ubalozi rasmi na kusaidia kuepusha sintofahamu, pamoja na kuomba ushirikiano na ushauri wao kuhusu fedha zozote zitakazochangishwa. Siku hiyo hiyo, DICOTA ilipokea barua pepe yenye majibu ya kutia moyo kutoka kwa Mh. Balozi Masilingi, na baadae pia kutoka kwa Mh Balozi Mbega, kuishukuru DICOTA na kuitakia mafanikio katika Kampeni hii. Majibu haya ya haraka yaliipa DICOTA nguvu ya kutamka kuwa imejulisha Wawakilishi wetu husika..
  • Aprili 14, DICOTA iliomba barua rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania hapa Marekani kutambua Kampeni hii, badala ya kuchapisha na kusambaza barua pepe ambazo imekuwa ikipokea. Nia ilikuwa kuweka wazi mawasiliano ya DICOTA, pamoja na kuepuka sintofahamu na kutoa hofu kwa watakaoguswa kuchangia kampeni hii.
  • Aprili 15, DICOTA ilipokea barua kutoka Ubalozi wa Tanzania, Marekani, kusikitika kwamba hautoweza kutoa utambulisho rasmi kwa Kampeni, wala kuhusika kwa namna yoyote kuchangisha fedha. Barua hiyo iliyoelekezwa kwa Mwenyekiti wa Bodi ya DICOTA, ilichapishwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii mnamo Aprili 17.

Kama ilivyokusudiwa awali, Ubalozi wa Tanzania Marekani hautachangisha au kuratibu matumizi ya fedha zozote.

DICOTA, itaendelea kusimamia fedha zote zitakazochangishwa kupitia kampeni ya “Dhibiti Mlipuko: COVID-19 Tanzania”, na itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa umakini kudhibiti janga la COVID-19 Tanzania. Itaendelea kushirikiana kwa karibu na wawakilishi wa Serikali waliopendekezwa na Idara ya Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje. Baada ya Kampeni, DICOTA itatoa ripoti makini ya fedha zote zilizochangwa, pamoja na matumizi yake.

DICOTA inatoa pole kwa waTanzania diaspora ambao wameathirika kwa namna moja ama nyingine kutokana na janga hili la COVID-19, na itaendelea kushirikiana na viongozi wa jumuiya zetu kusaidiana kwenye janga hili kama ilivyo desturi na wajibu wetu kama waTanzania. Aidha, DICOTA, itaendelea kutoa elimu na kujibu maswali ya jamii kuhusu janga la COVID-19 kupitia majadiliano ya kila wiki, pamoja na wataalamu walio mstari wa mbele kukabiliana na janga la COVID-19 duniani, ikiwemo Tanzania.

DICOTA, inawasihi waTanzania popote walipo kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Coronavirus na kujikita mapambano dhidi ya janga la COVID-19, ambalo ni tishio duniani kote, hata hapa Marekani. DICOTA inatanguliza shukrani za dhati kwa wote walioguswa tayari na watakaoguswa kuchangia Kampeni hii ya “Dhibiti Mlipuko: COVID-19 Tanzania”.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Dr. Frank Minja
Rais, DICOTA

Bi Asha Nyang’anyi
Mwenyekiti wa Bodi, DICOTA